BIDAA NA VIPENGELE VYAKE
Baadhi ya vipengele vya Bid’ah ni kama vifuatavyo:
1. Kila bid’ah ni Dhwalaalah.
Kilugha
Bid’ah ni kitu chochote kipya au kitu ambacho hakijafanywa kabla,
yaani, hakina mfano kabisa wa mbeleni. Katika muono wa kisheria, kila
Bid’ah ni Dhwalaalah na hakuna Bid’ah hasanah au sayyi’ah (Bid’ah nzuri
na mbaya). Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema
katika hadith, “Kullu Bid’atin dhwalaalah wa kullu dhwalaalatin fin naar (kila Bid’ah ni Dhwalaalah na kila Dhwalaalah ni motoni)” (Imepokewa na Imam Ahmad, Abu Dawud, at-Tirmidhy na wengineo).
Dhalalah
ina maana ya kwenda kombo au kufuata njia ya upotevu na kwenda kinyume
na ukweli. Tukitazama Qur-aan, tutaona vipi Allaah (Subhaanahu Wa
Ta'ala) ametumia neno hilo
‘dhwalaalah’ au ‘dhwaal’. Neno hili linatumika kwa mtu anayefanya
dhambi au anafanya kosa katika mambo ya kidini lakini na pia linatumika
kwa wale watu ambao wamepotea kutoka kwa njia nyoofu au wale walioigawa
dini. Kwa mfano katika Suratu Faatihah (Sura ya kwanza), neno
lililotumika ni ‘Dhaaliin’ halikutumika kwa wafanyao madhambi pekee
lakini limetumika kwa watu waliopotea kutoka kwa ile njia ya sawa, yaani
Wakristo. Hivyo pale Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
alipoielezea bid’ah, alitumia neno kali sana kwa upotevu huo, yaani dhalalah, kama alivyosema, “Kulla bid’atin dhwalaalah (kila bi’dah ni dhwalaalah)”. Hakusema kuwa kila bid’ah ni dhambi au ni kosa lakini kwa hakika ni jambo ambalo ni kubwa kuliko hilo. Huu ni upotevu, jambo ambalo linamtoa mtu katika Swiraatul Mustaqiym (njia ilinyooka).
2. Bid’ah inafanywa kama njia ya kumridhisha na kuja karibu na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala).
Kwa
maneno mengine, yeyote anayefanya bid’ah, anadai kwa kufanya hivyo
atakuja karibu na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala). Hii ni tofauti kabisa
na kufanya dhambi kama
alivyosema Imam Ahmad Ibn Hanbal, “Mkosefu mkubwa (fasiq) katika
msimamo wa Ahl-Sunnah Wal Jam’ah ni bora kabisa kuliko mchaji Allaah
miongoni mwa Ahl-Bid’ah (watu wa Bid’ah)”. Mwenye kufanya dhambi
(mkosefu), kwa uchache, anajua ya kwamba chochote afanyacho ni makosa na
wala hadai kuwa hilo
ni halali na kuwa analifanya ili kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa
Ta'ala). Hata hivyo, yule anayefanya bid’ah sio tu anakwenda kinyume na
Qur-aan na Sunnah lakini bado anadai ya kwamba anayofanya ni sawa na
anafanya hivyo ili kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na ni njia
ya kumleta karibu zaidi Naye (Allaah). Na huu ni uwongo mkubwa zaidi
ambao mtu anafanya kwa kusema kuwa kitendo hiki kinamridhisha Allaah na
hana dalili kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) kwa dai lake hilo.
Hivyo,
sehemu ya wazo hili la bid’ah ni kuwa yule mwenye kufanya hudai kwamba
linakubaliwa na dini pamoja na Sheria na ni lenye kumpendeza Allaah
(Subhaanahu Wa Ta'ala). Hii ndio nukta inayogawanya baina ya bid’ah na
jambo lisilokuwa bid’ah.
3. Bid’ah inaweza kuwa kuanzisha kitendo kipya na pia kukibadilisha kitendo kilichokuwepo mwanzo.
Maana
yake ni, pale mtu anapoanzisha kitendo kipya huku akidai kuwa kitendo
hicho kimekubaliwa na Sheria bila dalili yeyote ni bid’ah. Kwa namna
hiyo hiyo, pale mtu anapoacha kitu Fulani akidai kuwa kwa kuacha kitu
hicho basi anamridhisha Allaah na hana dalili yeyote kutoka kwa Qur-aan
au Sunnah, hiyo pia inakuwa bid’ah. Kwa mfano, wakati wa Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuja watu watatu katika nyumba
zake na kuwauliza wakeze kuhusu Ibadah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam), walipoelezewa waliona ni kama kidogo sana.
Hivyo wakajipangia jinsi watakavyofanya Ibadah zao, mmoja akasema yeye
ataswali usiku kucha, na mwengine akasema yeye atafunga kila siku na wa
tatu akasema kuwa yeye hataoa. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) alipoambiwa habari hiyo alikwenda kwa hawa watu watatu na
kuwauliza je, ndio nyinyi muliosema kadha na kadha nao wakajibu ndio. Na
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya haraka
kuzikemea na kuzikataza bid’ah hizi ambazo zinaonekana ni nzuri (huenda
sisi tukadhania na kufikiria je, kutakuwa na makosa ya mtu kumuabudu
Allaah kwa wakati wote?). Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaeleza hawa watu kuwa
yeye anamcha Allaah zaidi kuliko wao na ana taqwa ya daraja ya juu
lakini anaswali na kulala, anafunga na kula na ameoa wake (sio mke
mmoja). Na akamalizia kwa kusema yeyote atakayekengeuka na Sunnah zake
basi si katika mimi (yaani si pamoja na Mtume [Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam])
{Hadithi hii imepokewa na al-Bukhari na Muslim kutoka kwa Anas bin
Maalik [Radhiya Allaahu 'anhu]}. Hapa ukitizama katika watu hawa watatu,
wawili wa kwanza walikuwa tayari kuongeza Ibadah zao zaidi na zile
ambazo zipo katika sheria na wa tatu akataka kuacha Ibadah ya ndoa
ambayo ipo katika sheria na iliyokubaliwa na Allaah (Subhaanahu Wa
Ta'ala). Huyu wa tatu alikuwa ataka kujifananisha na makasisi wa
Kikiristo au watawa wao na pia kama masufi Waislamu ambao wanadai ya
kwamba wanafanya hivyo kumridhisha Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) na huu
ukawa ni uzushi na kinyume na Uislamu.
4. Kila kitu katika Sheria kinaweza kuwa na bid’ah inayotengenezwa au kuhusiana nayo.
Sheria
imejumlisha itikadi, ibadah na biashara au muamala na watu. Hivyo,
bid’ah si mambo katika itikadi pekee au mambo ya ibadah lakini inaweza
kuwa hata katika biashara na muamala. Kwa mfano, ikiwa mtu atadai ya
kwamba kunahitajika mashahidi wanne katika mapatano ya kibiashara na
wala sio wawili kama ilivyowekwa na Uislamu hivyo atakuwa ametupa mipaka ya kisheria na kuangukia katika bid’ah.
5.
Bid’ah haina dalili katika Qur-aan, Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) wala haikukubaliwa na Ijmaa (kongamano) ya
Masahaba.
Mfano maarufu ambao unatajwa na watu wa bid’ah (Ahl-Bid’ah) katika yale matamanio yao
ya kufanya aina Fulani za bid’ah ziwe halali, ni ule mfano wa ‘Umar
(Radhiya Allaahu 'anhu) kuifanya Swalah ya tarawehe itekelezwe kwa
jamaa. Wanadai ya kwamba Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alianzisha
tarawehe ya kila siku katika Ramadhaan ambapo Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) alitekeleza hilo
kwa muda wa siku 3 pekee, na ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema ya
kwamba ameanzisha bid’ah nzuri, tunaweza kukubali fikra hii ya bid’ah.
Hata hivyo, huku ni kufeli (kushindwa) kutofautisha baina baina ya maana
ya bid’ah kilugha na maana yake ya ki-istilahi (yaani maana ya
kisheria).
Kwa
mfano Allaah katika Qur-aan Anatuelezea kuhusu Sunnah Zake. Bila shaka
ni kuwa yeyote anapotaja kuhusu sunnah, inarudi kwa sunnah za Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na vipengele vyake vya
kisheria. Hivyo hivyo pale ‘Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alipotaja hizi
Swala za tarawehe za kila siku, alikuwa anamaanisha ile maana yake ya
kilugha. Dalili ya dai hili lipo wazi kabisa. Swala ya Tarawehe haikuwa
ni jambo geni katika dini. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) alianzisha swalah hizi, na sababu ya pekee iliyomfanya yeye
aache inaelezwa wazi katika hadithi zake ya kwamba hataki Ummah wake
upate shida kwa swalah hiyo kufanywa faradhi. Hata hivyo, alipofariki
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), risala ya Uislamu
ilikuwa imekamilishwa na swalah ya tarawehe itakuwa daima ni yenye
kuhimizwa kwa kiasi kikubwa na wala sio faradhi. Hivyo, ‘Umar (Radhiya
Allaahu 'anhu) alianzisha tu kitendo ambacho tayari kilikuwa ni sunnah
na wala sio kuanzisha sunnah. Na pia ile sababu ya kutoswaliwa kwa jamaa
iliondoka baada ya kuaga dunia kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam), hivyo hakukukuwa na aina yeyote ya uwezekano wa
kuteremshwa wahyi. Na matendo ya makhalifa waongofu pia ni katika sunnah
(tizama Hadithi nambari 28 ya al-Arba‘iina an-Nawawiyyah).
Kuhitimisha
sehemu hii ya makala haya, ni lazima ieleweke ya kwamba bid’ah si jambo
tu jipya ambalo limeanzishwa katika dini kwa dai la kumridhisha Allaah
(Subhaanahu Wa Ta'ala), lakini kwa yule mwenye kuanzisha na yule mwenye
kufuata bid’ah kwa hakika anatuhumu ya kwamba dini ina upungufu. Hakika
ni kuwa wao wanatuonyesha ya kwamba zipo njia za kuja karibu na Allaah
(Subhaanahu Wa Ta'ala) pamoja na kumridhisha ambako hakupatikani katika
Qur-aan au Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na kuwa wao wana njia ya kuamini au kufanya amali na kumuabudu Allaah
ambako kunampendeza Yeye na njia mzuri zaidi kuliko zile zilizofundishwa
na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwamba hii dini
ya Uislamu iliyokamilika ina upungufu na hiyo ndio sababu iliyowafanya
wao kuongeza baadhi ya vitu au dini hii ina vitu vingi sana
na hiyo ndio sababu ya wao kupunguza baadhi ya mambo. Huku
(Naudhubillahi) ni nkumtusi Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) kusema ya
kwamba hakuweza kumkamilishia na kumfundisha Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa njia bora na hivyo ilibidi watafute wao
wenyewe njia nzuri. Hii ni kukana kauli ya Allaah Mwenyewe katika
Qur-aan:
{Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini}. (5:3)
Na huko ni kukana kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: “Hakuna
kitu ambacho kitakuleta karibu na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) kuliko
yale niliyowaambieni kufanya na hakuna kitakacho wapeleka nyinyi mbali
kuliko kufanya yale niliyowakatazeni kufanya”.
Hivyo,
tunatakiwa kuchukia bid’ah. Hiki ndicho kiini cha mambo. Uchukivu huu
ni kuonyesha mapenzi yetu kwa Allaah na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) na pia kuipenda dini hii ambayo tunajua na kuwa na
yakini kuwa ndio iliyo sahihi kabisa na itabaki hivyo mpaka siku ambayo
Allaah Ataibadilisha ardhi hii kwa nyengine.
Madhara (Hatari) ya Bid’ah:
Kama
bid’ah ingebanwa kwa yule mwenye kufanya pekee basi huenda
hatungefadhaishwa au kubabaika kama tulivyo sasa, lakini hakika ni kuwa
hatari za bid’ah na yale madhara na maafa yake yanasambaa kutoka kwa mtu
anayefuata na kuwafikia watu wanaoishi naye na mwishowe kwa Ummah
mzima. Hivyo, dini kwa ujumla inaathirika kwa ajili ya bid’ah zao na
uasi wa kidini. Wanachuoni wametoa kauli mbalimbali na kuuliza maswali
mbalimbali kama haya na kuyapatia ufumbuzi, “Kwa nini Uislamu umeupiga
vita vikali jambo hili la bid’ah? Kwa nini Uislamu umeichukulia bid’ah
kuwa ni Dhalalah? Kwa nini imemchukulia mwenye kuifanya kuwa ataingia
Motoni? Kwa nini Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
ametuonya vikali sana kuhusu jambo hilo?” Baada ya maswali haya ametoa majibu kwa nini bid’ah imepingwa vikali sana. Hatari zinazotokana na bid’ah ni kama zifuatazo:
1. Mzushi anajiweka katika cheo cha kutunga sheria:
Uhakika ni kuwa Uislamu umetuonya sana na bid’ah kwa sasa mzushi anaiweka nafsi yake katika cheo cha Allaah. Na ya kuwa yeye anajua asiyojua Allaah, kama
kwamba anasema: “hakika yale uliyotuletea hayatutoshi, hivyo sisi
tunazidisha juu ya yale ulituteremshia”. Hivyo anajiweka katika daraja
ya kutunga sheria na kujipatia haki ya kuweka sheria. Utungaji wa sheria
kwa hakika ni haki ya Allaah pekee. Qur-aan inatueleza:
أَمْ لَهُمْ شُرَكَاء شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّهُ
“Au hao wana miungu ya kishirikina walio watungia dini asiyo itolea idhini Allaah?”
(42: 21)
Na
kutunga yale yasiyoidhinishwa na Allaah ni hatari kubwa kwa kuwa
mwanadamu ameijaalia nafsi yake kuwa sawa na Allaah Aliyetukuka. Na
anaona kuwa ni haki yake kuzidisha katika dini ya Allaah, na huu ni
mlango ambao huleta hatari kubwa ambayo huwapelekea watu katika shirki
na hili ndilo jambo lililoharibu dini kabla.
Dini
nyinginezo zilihalalisha nini? Zilihalalisha bid’ah kwa kuifungulia
milango na wakajipatia ruhusa na haki ya kuongeza mambo katika dini ya
Allaah na wakawapatia haki hiyo makasisi wao au watawa wao. Hivyo dini
ikawa si dini na hili ni jambo ambalo Uislamu umelipiga vita vikali,
pale Allaah Aliposema:
اتَّخَذُواْ
أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللّهِ وَالْمَسِيحَ
ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُواْ إِلاَّ لِيَعْبُدُواْ إِلَـهًا وَاحِدًا
لاَّ إِلَـهَ إِلاَّ هُوَ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ
“Wamewafanya
makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni marabi badala ya Allaah, na pia
Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipo kuwa wamuabudu Mungu
Mmoja, hapana mungu ila Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayo
mshirikisha nayo” (9: 31).
'Adiy
bin Haatim (Radhiya Allaahu 'anhu) aliposilimu baada ya kutoka katika
Ukristo (ambao alikuwa akiufuata wakati wa Ujahiliyyah) alikuja kwa
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa
anaisoma aya hii: (9:31). Alisema: “Hakika wao hawawaabudu”. Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Bali wanawaabudu, kwani wao huwaharamishia halali na kuwahalalishia haramu nao wakawafuata, na kufanya hivyo ni kuwaabudu”
(Imepokewa na Ahmad, at-Tirmidhy na Ibn Jariir). ‘Adiy alifahamu Ibadah
ni zile taratibu za dini (au taratibu fulani za ibadah) tu kwa mfano
swalah, kurukuu, kusujudu na mfano wake. Na hapa Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) alimfahamisha ya kwamba sio dharura kufanya
hivyo, kwani ibadah ina maana pana zaidi. Ibadah ni twaa ya daima kwa
yale wanayofanya, yale wanayoharamisha na wanayohalalisha na mengineyo
katika mambo ya dini ni ibadah, kwani ni Mola ambaye ana haki ya
kuhalalisha na kuharamisha. Yeye (Allaah) ndiye mwenye haki ya kuabudiwa
wala si kinyume ya hayo.
Mzushi hivyo anajipatia cheo cha kutunga sheria na kujiweka sawa na katika upinzani na Allaah Aliyetukuka.
2. Mzushi anaona kuwa dini ina upungufu, hivyo kutaka kuikamilisha:
Watu
wa bid’ah wanaona upungufu katika dini nao wakawa wanafanya juhudi ya
kuikamilisha katika zile kasoro. Lakini ni jambo ambalo linafahamika na
kila Muislamu na hata asiyekuwa Muislamu ya kwamba dini ya Uislamu
imekamilika na AllaAh Ametutimizia neema Yake kwa kutukamilishia.
Anasema
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الإِسْلاَمَ دِينًا
“ Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini” (5: 3).
Imam
Maalik (Imam wa ardhi ya Hijrah) alisema: “Yeyote atakayezua katika
Uislamu bid’ah ambayo anaiona ni nzuri amedai ya kwamba Mtume Muhammad
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya hiyana katika
kutekeleza ujumbe, kwani Allaah Aliyetukuka anasema, ‘Leo
nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na
nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini’. Hivyo chochote ambacho
hakikuwa dini wakati huo hakiwezi kuwa dini sasa”.
Uzushi
katika dini unakuwa ni wenye kumtuhumu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) kuwa hakutekeleza jukumu aliloletewa nalo na Allaah.
Na Allaah Anasema:
يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ
“Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako . Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake” (5: 67).
Dini
imekamilika na hivyo haina haja ya kuzidishwa mambo kwani
kilichokamilika hakikubali ziada kwa hali yeyote. Kitu chenye upungufu
ndicho ambacho kinaweza kuongezwa. Hapa walisimama imara kabisa Masahaba
na Maimamu wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah na waliowafuata kwa wema dhidi
ya bid’ah kwani huko ni kuituhumu dini kuwa imepungua na kumtuhumu Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amefanya hiyana.
3. Bid’ah inaifanya dini kuwa nzito na inaitoa katika maumbile yake ya wepesi na usahali:
Dini ambayo imeteremshwa na Allaah ni nyepesi na akatumwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)mwongofu na usahali, uwongofu katika itikadi na wepesi katika taklifu za amali. Allaah Anasema:
يُرِيدُ اللّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ
“Allaah Anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito” (2: 185)
na pia:
وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ
“Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibraahiym” (22: 78).
Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakika mimi nimetumwa kufanya sahali mambo na wala sio kuleta uzito wowote” (Imepokewa na al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah).
Hivyo
dini imekuja na usahali kwa watu na wale wenye kuleta bid’ah wanaitoa
katika maumbile yake ya wepesi. Hivyo wanawapatia watu taabu na mashaka
na wanaongeza vitu ambavyo vinakuwa ni mizigo na minyororo na taklifu
kubwa kwa watu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
alikuja kuondoa hiyo mizigo na minyororo iliyokuwa juu ya watu (kwani
sheria za zamani zilikuwa ngumu). Allaah Anatufahamisha hayo katika
Qur-aan tukufu kwa wasifu wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) kama alivyotajwa katika vitabu vya mwanzo – Taurati na Injili:
الَّذِينَ
يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ
مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنْجِيلِ يَأْمُرُهُم
بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ
الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَآئِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ
إِصْرَهُمْ وَالأَغْلاَلَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ
Ambao
kwamba wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiyesoma wala kuandika, wanaye
mkuta kaandikwa kwao katika Taurati na Injili, anaye waamrisha mema na
anawakanya maovu, na anawahalalishia vizuri, na ana waharimishia viovu,
na anawaondolea mizigo yao na minyororo iliyo kuwa juu yao” (7: 157).
Na Allaah Ametufundisha dua ambayo iko mwisho wa Suratul Baqarah ambayo inasema:
رَبَّنَا
لاَ تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا رَبَّنَا وَلاَ تَحْمِلْ
عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا
رَبَّنَا وَلاَ تُحَمِّلْنَا مَا لاَ طَاقَةَ لَنَا بِهِ وَاعْفُ عَنَّا
وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَآ أَنتَ مَوْلاَنَا فَانصُرْنَا عَلَى
الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ
Hawa
watu wa bid’ah wanataka kurudisha ugumu wa dini zilizotangulia katika
Uislamu na wanataka kuongeza taklifu ambazo zitakuwa mzigo kwa watu na
hivyo kuleta uzito usiotakikana. Taklifu za dini ni sahali na nyepesi sana, kwa mfano: Allaah Anasema:
إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا
“Hakika Allaah na Malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi mlio amini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu” (33: 56).
Na
namna bora ya kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) ni ile aliyotufundisha mwenyewe (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam): “ALLAAHUMMA SWALLI ‘ALAA MUHAMMADIN WA ‘ALAA AALI MUHAMMAD…” (Imepokewa
na al-Bukhaariy na Muslim kutoka kwa Ka‘b bin ‘Ujrah (Radhiya Allaahu
'anhu) Kusema hii Swala ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) inaweza kuchukua dakika ngapi?
“Wanakuja
watu ambao wanaongeza maneno katika Swalah ya Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) namna ambayo ina taklifu kubwa sana
ambayo haikuteremshwa na Allaah wala Mtume Wake. Nilikuwa nikiwaona
watu wa kawaida wakisoma bila ya kufahamu chochote. Na dua nyingine
ambazo zimeanzishwa na watu ni zile nyiradi na hizbu ambazo nilipokuwa
mdogo nilikuwa nikiwaona watu katika msikiti kabla ya Alfajiri wakisoma.
Nilikuwa nawaona baadhi ya watu wakihifadhi nyiradi hizo zilizokuwa
zikiitwa ‘Uradi wa al-Bakari’ na hii ni dua inayofuata herufi za
Kiarabu. Dua inaanza na herufi ya hamzah, kisha ba mpaka mwisho. Na
ulikuwa ukiwauliza kuhusu maana walikuwa hawajui kabisa! ” (As-Sunnatu wal Bid’ah, uk. 30 – 31).
Ewe
ndugu yangu katika Imani! Je, kuna dua iliyo nyepesi, nzuri na sahali
kuliko dua ambazo zipo ndani ya Qur-aan au Sunnah za Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Dua ya Qur-aan mfano wa:
رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ
“Mola wetu , tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde na adhabu ya Moto!” (2: 201).
Kwa nini tunafanya mambo yawe magumu kwa watu kwa kuwahifadhisha hizo dua badala ya kuwahifadhisha mfano wa dua hii ya Qur-aan?
Mwandishi
wa kitabu hicho cha As-Sunnatu wal Bid'ah anatoa mfano mwengine: “Mara
moja nilimwuliza mtu, kwa nini huswali? Akanijibu ya kwamba: ‘Sijui
kushika wudhu’. Nikamwambia: ‘Hujui kuosha uso, mikono miwili, kupaka
kichwa na kuosha miguu miwili?’ Akasema: ‘Hayo ninajua, lakini
sijahifadhi yale yanayosemwa mtu anapoanza kushika wudhu (kutawadha)’.
Hiyo ni kusema unapoanza: ‘Alhamdulillahi alladhi ja’alal maa ….’
Unapotia maji puani, ‘Allaahumma arhamni biraihatil jannah …’ Unapoosha
uso, ‘Allaahumma bayyidh wajhii…’ na kadhalika mpaka kumaliza. Kila kitu
wamekiwekea dua na mtu wa kawaida anaona ili wudhu kuwa sawa ni lazima
ulete dua zote hizo ili swalah ipate kusihi. Kwa nini yote haya?”
Nakumbuka nilipokuwa mtoto jinsi ganii katika kisiwa cha Lamu wakati wa Ramadhani watu walivyokuwa wakisumbuka sana
kutekeleza amri ya funga kwa kungojea mpaka saa nne au tano ili mwalimu
fulani awatilishe watu nia kwa kutumia microphone. Hata mtu akiwa na
usingizi namna gani ilikuwa ni lazima angoje mpaka wakati ufike na lau
atalala basi saumu yake haiswihi. Na saa nyengine watu walikuwa
wakimngojea shekhe fulani kwani wanapofunga kwa kunuwizwa naye basi
funga inakuwa sahali. Ikiwa atakuwa mwengine basi itakuwa na taabu.
Mpaka sasa katika baadhi ya vitongoji watu ambao kwao hakuna Msikiti
inabidi watembee masafa ya kilomita kadha kwenda kuswali Ishaa sehemu
ambayo ina Msikiti ili wapate kutilishwa nia. Kuna baadhi ya vitongoji kama vya Taita-Taveta (Kenya) na Arusha (Tanzania) au Tanga ambako mwanamke ili kujitahirisha mpaka aogeshwe na mwalimu au shekhe. Laa hawla wala quwwata illa billahi!!
Uislamu ulisimama imara dhidi ya bid’ah ili watu wasiingie katika mambo mazito na kuongeza vitu ambavyo vitakuwa juu sana
na yale yaliyoteremshwa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala). Natija yake
ni kuwa watu watakuwa na mzigo mkubwa wa taklifu ambazo zitawapatia
dhiki kubwa katika utekelezaji wa mambo ya dini.
4. Bid’ah katika dini zinaua (zinaondosha) Sunnah.
Imepokewa
kutoka kwa salaf saalih ya kwamba: “Hakuna watu ambao watahuisha bid’ah
isipokuwa huondoka mfano wake katika Sunnah”. Hivyo ni kitu
kinachoeleweka kuwa hakutaanzishwa bid’ah isipokuwa huchukua nafasi ya
Sunnah. Au watu huongeza katika Sunnah mpaka Sunnah ikawa haitekelezwi
katika njia yake sahihi. Ibn Abbas anasema, “Pindi bid’ah inapoanzishwa
basi Sunnah hutoweka na hii huendelea mpaka bid’ah ikabakia na Sunnah
ikatoweka kabisa”. Hasan Ibn Attwiyah, mmoja wa Tabii alisema: “Watu
wanapoikubali bid’ah, Allaah huondosha Sunnah kutoka kwao na hairudishi
mpaka Siku ya Kiyama”.
Na hili ni jambo la kawaida, nayo ni kanuni, kanuni ya kilimwengu, kanuni ya kijamii. Kama
alivyosema msemaji ya kwamba: “sijaona israfu (ubadhirifu) ukifanywa
isipokuwa kuna haki zinazokiukwa. Hivyo, mwanadamu anapotumia nguvu zake
katika bid’ah, ni lazima nguvu hizi zitaiathiri Sunnah kwani mwanadamu
juhudi zake zina kikomo”. Hivyo, utawaona wazushi wanashinda katika
mambo ya bid’ah lakini wanapoteza Sunnah. Anaelezea Shaykh wa
Misr yaliyomfika alipokuwa akisoma sekondari katika chuo cha al-Azhar
(Misri) katika mji wa Twanta. Na hiki kijiji cha Twanta alikuwa akiishi
As-Sayyid al-Badawi ambaye ni maarufu. Na huko kulikuwa na mashekhe
ambao kila wakati (mchana na usiku) walikuwa wakikaa ubavuni mwa
al-Badawi. Wakati mmoja nilijadiliana na shekhe wangu ambaye alikuwa
fakihi wa Kihanafi, lakini alikuwa katika kikundi ambacho kinawatukuza
mawalii. Huyu shekhe alikuwa akitufundisha mlango wa kuchinja katika
Fiqhi, nami nilikuwa napenda kufunganisha Fiqhi na maisha. Nilimwambia:
“Ewe shekhe wetu! Watu wameisahau Sunnah hii na hivyo wenye kuchinja
wamekuwa kidogo sana.
Itikadi yangu ni kuwa lau mashekhe wataitilia mkazo basi watu huenda
wakaihuisha sunnah hii”. Akasema shekhe: “Uwezo wa watu wa kifedha
umekuwa mdogo”. Nikasema: “Lakini katika sherehe nyengine watu
wanachinja na hiyo si katika sunnah”. Akasema: “Unamaanisha nini?”
nikasema: “Ninamaanisha kuwa wao huchinja katika maulidi (kuzaliwa) kwa
as-Sayyid. Pindi wakati huo ukifika huchinjwa mbuzi na kondoo maelfu kwa
maelfu lakini katika Iidul Adh’ha (Idi ya Kuchinja) hapatikani mwenye
kufanya hivyo. Lau mashekhe wangezungumzia jambo hili na kuirudisha
sunnah badala ya kumchinjia Sayyid, wachinje katika Idi kubwa na hivyo
watakuwa wamehuisha sunnah. Na hata kama hawatatoa sadaka kwa kitu chochote ile hali ya kumwaga damu pekee ni katika kutekeleza wito wa Uislamu kwani Allaah Amesema:
فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ
“Basi swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako ” (108: 2)”.
Sikumaliza
haya maneno isipokuwa nilimuona shekhe amenikasirikia na kunitoa katika
darasa na akaniona mimi ni mtu wa kuleta vurugu na kuwa mimi
ninawachukia mawalii na watu wema!
Hii
ilinikumbusha mimi ya kwamba hakuna watu wanaohuisha bid’ah na
kujishughulisha nafsi zao isipokuwa wanaua sunnah mfano wake na hii ndio
siri katika kupinga bid’ah.
Hivyo,
bid’ah inaleta chuki kwa Sunnah. Ahl-Bida sio tu wanakataa kuikubali
Sunnah sahihi bali pia wanajikataza kwenda katika msikiti au sehemu
ambazo Sunnah hutekelezwa.
5. Bid’ah zinaleta mfarakano katika Ummah na kuondoa umoja wao.
Nayo
ni kusimama imara katika kutekeleza Sunnah inaleta umoja wa Ummah juu
ya kauli moja na hili linawanya Waislamu kuwa safu moja. Lakini bid’ah
haimaliziki. Haki ni moja tu lakini batili ina rangi nyingi na aina
tofauti. Njia nyoofu ya Allaah ni moja lakini vinjia vya shetani ni
vingi sana. Na hivyo imekuja katika hadithi ya Ibn Mas‘ud (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituchorea mstari. Kisha
akasema, ‘Hii ndio njia ya Allaah’. Kisha akachora mistari kuliani na
kushotoni kwake na akasema: ‘Hizi ni vijia, katika kila njia kuna
shetani ambaye anawaita watu katika njia hiyo’. Hapo akasoma:
وَأَنَّ
هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ
فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ
تَتَّقُونَ
“Na
kwa hakika hii ndiyo Njia yangu Iliyo Nyooka. Basi ifuateni, wala
msifuate njia nyingine, zikakutengeni na Njia yake. Haya amekuusieni ili
mpate kuchamngu” (6: 153).
{Imepokewa na Imam Ahmad, at-Tabari na al-Haakim ambaye ameisahihisha na kukubaliana naye adh-Dhahabiy}.
Na hivyo Ummah huu uliposhikilia sunnah ilikuwa kauli yao
moja na mfarakano ulipokuja ummah huu uligawanyika makundi tofauti.
Watu walitoka katika mfumo wa dini, baadhi ya mambo yakiwa ya bid’ah
katika itikadi ambayo yalifikia daraja ya ukafiri, mfano wa wale ambao
wanakataa ya kwamba Allaah Anajua kila kitu au Allaah Alikuwa hajui
mambo mengine kabla. Hawa ni wale watu ambao Ibn ‘Umar alijitenga nao na
akasema: “Lau mmoja wao atakuja na amali mfano wa mlima Uhud
haitakubaliwa na Allaah Aliyetukuka”. Na kuna wengine waliomfananisha
Allaah na viumbe vyake. Na kuna wale wanaokataa uwezo wa Allaah lakini
hawakatai elimu ya Allaah. Na kuna wale waliowakufurisha Waislamu na
wakahalalisha kuuliwa kwao mfano wa Khawaarij wakati wa Khalifa 'Aliy
(Radhiya Allaahu 'anhu) na baadaye mbali na kuwa walikuwa wanafanya
ibadah nyingi.
Masahaba
wote walikuwa msitari wa mbele katika kufuata sunnah za Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Walikuwa wanapendana na wakati
walipokuwa na tofauti ya ijtihadi baada ya ‘Uthman (Radhiya Allaahu
'anhu) walibaki katika mahaba baadhi yao
kwa wengine. Japokuwa kulitokea vita katika baadhi ya vipindi hasa kile
cha Ali (Radhiya Allaahu 'anhu) lakini walibaki kupendana na
kushirikiana na hata kuswali katika misikiti ya wenzi wao bila ya chuki.
Hata hivyo, Makhawaarij walitoa rai zao katika Vita vya Siffin baina ya
Mu‘awyiah na ‘Ali (Radhiya Allaahu 'anhu), Waislamu waligawanyika
katika msimamo wa Ahl-us-Sunnah na hivyo kuwa watu wa kwanza wa bid’ah.
Katika kikundi hiki hakukuwa na sahaba hata mmoja aliyejiunga, na ‘Ali
(Radhiya Allaahu 'anhu) alimtuma Ibn ‘Abbas (Radhiya Allaahu 'anhu)
kuzungumza nao na wengi wakatoka wakatoka katika kundi hilo la Khawaarij na kurudi chini ya Uongozi wa Ali (Radhiya Allaahu 'anhu) ).
Ummah
lau utaachiwa watu wa bid’ah basi hauwezi kuja pamoja, lakini unakuja
pamoja tu wakati utasimama nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) kwa kufuata Kitabu cha Allaah na Sunnah Zake.
6. Bid’ah ni daraja la kuelekea kwenye Ukafiri:
Mwanachuoni
mmoja mkuu, Al-Barbahaari, mmoja wa wanafunzi wa Ahmad Ibn Hanbal,
alisema, “Tahadharini bid’ah, kwa sababu kila bid’ah iliyoanzishwa
inaanza kama
kitu kidogo na inafanana na ukweli na hivyo kuwadanganya watu. Watu
wanaanza kuifuata na hivyo kuwa kubwa na watu kunaswa na kuwatoa katika
Uislamu”.
Ibn Taymiyyah ameandika kipande kizuri sana
katika vitabu vyake kwa kuonyesha kuwa: “Kwa hakika, ukafiri wa
Mayahudi na Manasara ni kwa sababu ya bid’ah. Walikuwa wanaanzisha mambo
mapya katika dini na mambo yaliwachukua nje kabisa ya ujumbe wa sawa wa
Musa na ‘Isa Alaihima Salam”.
7. Kwa Ummah wa Kiislamu kwa jumla, bid’ah inarudisha nyuma kuenea Uislamu na Da‘wah kwa ajiili ya Allaah.
Njia
na rai za Ahl-ul-bid’ah zinatumiwa na maadui wa Uislamu kuuonyesha
Uislamu. Vipindi vingi katika runinga vinaufananisha Uislamu na dhikri
ya masufi, matendo ambayo yanakwenda kinyume na Uislamu. Wanaleta mambo kama
hayo ili kuwafanya watu waukimbie Uislamu kwa sababu ya itikadi hizo za
Ahl-ul-bida ambazo hazilingani na ‘fitra’ (maumbile). Ni kufuata
Uislamu wa kihakika pekee ndio watu wanaweza kuvutiwa kwani watu
huvutiwa na mambo ya kawaida yanaokwenda sambamba na maumbile ya
mwanadamu.
8. Kwa mtu binafsi, bid’ah inaharibu Akhira yake:
Chukua mfano wa mchwa ambao unaruhusiwa kuishi katika ubao. Bid’ah ina athari hiyo hiyo ya kama mchwa ambao hula ubao, nayo bid’ah hummaliza binadamu na kumuacha kama mkakasi. Kwa wakati wa karibu au mbali mtu kama
yule anaharibikiwa kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) ametuonya katika hadithi zake nyingi. Bid’ah itakataliwa na
Allaah na makazi ya mtu huyo yatakuwa ni motoni, kama
alivyotoa wasiya huo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
katika hadithi iliyopokelewa na Abu Daawuud na at-Tirmidhy. Allaah
(Subhaanahu Wa Ta'ala) ataweka kizuizi baina yake na tawba mpaka aache
bid’ah yake hiyo na arudi katika mafundisho sahihi ya Uislamu. Katika
ulimwengu ataona kuwa anafanya amali ya kujikaribisha na Allaah pamoja
na kumridhisha Yeye, lakini akhira, atakujakuta ya kwamba hana faida
yeyote kwa aliyoyafanya. Mzigo huu utakuwa mkubwa na hasa ikiwa alikuwa
akiwalingania wengine wafuate yale anayoyasema au kufanya, atakuwa na
mzigo mkubwa zaidi. Na wale wenye kufuata kiupofu pia watapata adhabu yao. Allaah (Subhaanahu Wa Ta'ala) anatuelezea hayo pale aliposema:
يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا
Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: ‘Laiti tungeli mt'ii Allaah, na tungeli mt'ii Mtume!’
وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا
Na watasema: Mola wetu ! Hakika sisi tuliwat'ii bwana zetu na wakubwa wetu; nao ndio walio tupoteza njia.
رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا
Mola wetu ! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana kubwa (33: 66 – 68).
Ufumbuzi wa kujitenga na Bid’ah:
Mwanzo
kabisa, watu wanaodai ya kwamba wanafuata Sunnah na kuwa katika msimamo
wa Ahl-us-Sunnah Wal Jama‘ah ni lazima waelewe na wafahamu hatari za
bid’ah na kuwa ni jukumu la kila mmoja kuchukia na kuipinga. Jambo
lolote likifanywa kinyume na Qur-aan na Sunnah ni wajibu wa Waislamu
kulikataza jambo kwa njia iliyo nzuri na kuwafahamisha watu madhara ya
kwenda kinyume. Kuna mtu aliyekuja kwa Imam Maalik na kumwambia kuwa
mimi nataka kuhirimia Madinah. Imam Maalik akamfahamisha kuwa kufanya
hivyo ni kinyume na Sunnah kwani ihramu (nia na vazi) inavaliwa katika
Miiqaat (sehemu maalumu zilizowekwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) Yule mtu akasema kuna tatizo gani na kwa sababu ya
umbali kutakuwa na thawabu zaidi. Imam Maalik akamsomea aya ifuatayo:
لَا
تَجْعَلُوا دُعَاء الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاء بَعْضِكُم بَعْضًا قَدْ
يَعْلَمُ اللَّهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا فَلْيَحْذَرِ
الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ
يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ
Msifanye wito wa Mtume baina yenu kama
wito wa nyinyi kwa nyinyi. Hakika Allaah Anawajua miongoni mwenu
wanaoondoka kwa uficho. Basi nawatahadhari wanaokhalifu amri yake, usije
ukawapata msiba au ikawapata adhabu chungu (24: 63).
Tuwaite watu kwa njia nzuri kwa busara na mawaidha mazuri. Allaah Anasema:
ادْعُ
إِلِى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ
وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن
ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ
"Waite
waelekee kwenye Njia ya Mola wako kwa hikima na mawaidha mema, na
ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako ndiye Anayemjua
zaidi aliyeipotea Njia Yake, na Yeye Ndiye Anayewajua zaidi walioongoka” (16: 125)
Hapana budi kuanzisha shughuli ya “Amru bil ma‘ruuf wa nahyun anil munkar” (kuamrisha mema na kukataza maovu). Bid’ah ni munkar mkubwa sana
na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia wazi
kabisa katika hadith ya kwamba ni lazima mtu aubadilishe (au aundoshe)
ule munkar kwa uwezo wake wote.
Ni
lazima tutumie fursa ya kuwaelimisha watu na kujifunga sisi wenyewe na
Sunnah za kweli za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na
kutambua mambo ambayo ni bid’ah na yale ambayo si bid’ah. Tufanye bidii
kuielewa Qur-aan na pia hadith za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam). Tujue imani ya kihakika na kufuata maagizo ya Allaah
na Mtume Wake. Na ikiwa tunampenda sana
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi tufuate mwendo
wake na kuacha kila ambacho si katika Sunnah zake. Allaah Anatuelezea:
Sema:
"Ikiwa
nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah atakupendeni na
atakufutieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye kufuta madhambi na
Mwenye kurehemu." (3: 31).
Tunamuomba
Allaah Atulinde tusiwe ni wenye kufanya bid’ah na Atuongoze katika njia
nyoofu na Atusaidie katika kujenga Imani zetu. Mazuri yote yanatokana
na Allaah na Mtume Wake na maovu na mabaya yote yanatokana na Shetani na
marafiki zake.
“Mola wetu ! Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Mola wetu ! Usitubebeshe mzigo kama ulio wabebesha wale walio kuwa kabla yetu. Mola wetu Usitutwike tusiyo yaweza, na utusamehe, na utughufirie, na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi tuwashinde kaumu ya makafiri” (2: 286).
No comments:
Post a Comment
add your comment here