Wednesday 24 August 2016

AL KAABA
 

IBADA YA HIJJA 

 UMRA

Nini Hijja?

Hijja, kilugha ni kukusudia; kisharia ni kukusudia kwenda Makka kutekeleza nguzo za Hija, tangu 'tawaf, sa'i (Safa na Marwa), kuhudhuria 'Arafa, na nguzo nyengine za Hija. Hutenda haya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kutafuta ridhaa zake.

Hukmu ya Hijja


Hija ni fardhi kwa kila mwenye uwezo, ni nguzo ya tano miongoni mwa nguzo tano za Uislam. Hija imekuja kwa Qauli ya wenyezi Mungu Mtukufu, qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na itifaqi ya Umma. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 "............Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea……". (Al 'Imraan : 97).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

 "Umejengwa Uislam juu ya (Nguzo) tano", (mpaka mwisho wa Hadithi).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  

 "Hijini kabla hamjakuwa hamuwezi kuhiji". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Mwenye kukanya kuwajibika Hija huwa amekufuru.


 

Fardhi Mara Moja


Wamekubaliana wanazuoni kuwa Hija ni fardhi mara moja katika umri. Al Aqra'i alimuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama Hijja ni kila mwaka? Mtume s.a.w. akasema:


 "Ni mara moja, mwenye kuongeza ni sunna".          (Imehadithiwa na Ahmad).

'Umra

Nini Úmra?


'Umra ni fardhi kama ilivyo Hija, ni fardhi kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:


"Na timizeni Hija na 'Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu……". (Al Baqara : 196).
Imepokewa kutoka kwa......


Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba alimuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama wanawake wanalazimika na Jihadi, akasema s.a.w.:

"Naam, Jihadi isiyo na vita ndani yake, Hijja na 'Umra".
Ameeleza Imam Al Tirmidhy r.a. kwamba Jaabir r.a. alimuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama 'Umra ni waajb, Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akajibu:  
 
 yaani, si waajibu, lakini ukifanya 'Umra ni kheri. Yenye kufanywa katika ibada ya 'Umra ni kama yale yenye kufanywa katika ibada ya Hija, lakini kwenye 'Umra hamna nguzo ya 'Arafa wala kulala Muzdalifa wala nguzo ya kulembea vijiwe (mawe), wala kuchija. 

Kujuwa Hukmu Za Hijja


Inampasa mwenye kutaka kwenda kuhiji ajifunze hukmu zote za Hija, yale ya waajibu, ya sunna, yenye kuruhusiwa na yale yenye kukatazwa na yale yenye kuba'tilisha Hija. Kujifunza ni waajibu, kwa sababu lenye kulazim kulifanya ni lazima kujuwa namna ya kulifanya. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui…". (Annahl : 43).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  

  "Kutafuta elimu ni fardhi (waajibu) juu ya kila Muislam mwanamume”          (Imehadithiwa na Al Bayhaqy)
Na katika riwaya nyengine: "Na Muislam mwanamke".

La Mwanzo Lenye Kupasa Kujifunza


La mwanzo lenye kupasa kujifunza ni kujuwa baina ya halali na haraam. Hivi ni kwa vile halali inasaidia katika kufanya mema na kujiepusha na maovu. Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwema, hapendi isipokuwa vyema. Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaamrisha Waumini yale yale aliowaamrisha Mitume a.s., amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaambia Mitume a.s.w.:

"Enyi Mitume! Kuleni vyakula vizuri na tendeni mema. ……". (Muuminun : 51).
Na amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaambia Waumini:

"Enyi mlio amini! Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni, ....". ( Al Baqara : 172)
Mwenye chumo la halali, hutakasika vitendo vyake; na asiekuwa na chumo la halali, inakhofiwa kuwa vitendo vyake huenda visikubaliwe.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
"…Hakika Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamngu". (Al Maidah: 27).
Amesema mshairi:

"Ukenda kuhiji kwa mali asili yake haraam, basi hukuhiji; amehiji mnyama (kipando chako)".
Hija ni miongoni mwa bora mno za a'amali, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:   
 "Bora mno ya a'amali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ni imani isiokuwa na shaka, na kupigana Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Hijja iliofanywa kwa ukamilifu na haikuingia ndani yake lolote lile lililokatazwa". (Imehadithiwa na Jama'a Wapokeaji Hadithi).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  
  "Mwenye kuhiji asiseme maneno machafu, atarejea kama alivyokuwa siku aliozaliwa na mama yake". (Imehadithiwa na Jama'a Wapokeaji Hadithi).
Hijja ni waajibu wenye kutekelezwa penye wasaa, lakini ni bora kufanya hima na haraka kuutekeleza mara ukipata uwezo, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Mwenye kumiliki mali na kipando cha kumfikisha kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu - Makka - na akawa asende kuhiji, basi hakuna juu yake isipokuwa kufa katika mila ya Kiyahudi au ya Kinasara". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Asiezuilika kutokana na maradhi, au haja ya hakika, au kuzuilika kutokana na mwenye madaraka (sultani, raisi, mfalme, n.k.) muovu; na akawa mtu huyo hakuhiji, basi akitaka naafe katika mila ya Kiyahudi au mila ya Kinasara". (Imehadithiwa na Ahmad).  ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment

add your comment here